Logo Design by FlamingText.com
Logo Design by FlamingText.com

HISTORIA YA DAMU AZIZI ULIMWENGUNI

Tukijukumbushe: “Siwezi, Sipaswi na Sitaki.” “Kwa Mungu ni lazima tufanye Mengi,
Upesi na Vizuri.”




Hii ni kati ya misemo maarufu iliyosemwa na Mtakatifu Gaspari katika
kipindi cha uhai wake hapa Duniani. Mtakatifu Gaspar tangu mwanzo aliamua kuwa mmisionari
na akashika msimamo huu hadi kuufikia utakatifu. Gaspar alifaulu kumwiga Kristo kwa
kulinganisha uhodari wa kibinadamu na neema ya Mungu. Wito wake uliojitokeza tangu
kuzaliwa kwake uliimarishwa na kukomazwa hadi upeo wa utakatifu kwa njia ya mazingira na
watu aliokutana nayo.
Mtakatifu Gaspar Del Bufalo alizaliwa huko Roma Januari 6, mwaka 1786; sikukuu Epifania
yaani Tokeo la Bwana, Gapar alizaliwa dhaifu, wakahofia angekufa hivyo akabatizwa siku
iliyofuata na akapewa majina ya mamajusi watatu watakatifu, yaani Gaspar, Melkiori na
Baltazari. Neema hiyo ya ubatizo ilikuwa chanzo cha maisha yake ya kipekee. Tangu hapo kila
mara aliitwa Gaspar. Wazazi wa Gaspar walikuwa Wakristo imara, baba yake aliitwa Antonio
Del Bufalo alikuwa mpishi katika jumba la kifalme; na mama yake ni aliitwa Anunciata
Quartieroni.
Mama Anunciata alikuwa Mchamungu na mfano wa kuigwa kwa wengi, aliyaimarisha maisha
ya Gaspar. Katika utoto wake wa miezi kumi na nane tu, Gaspar akiwa bado yu mtoto aliugua
ugonjwa wa ndui akawa kwenye hatari ya kuwa kipofu. Mama yake alimweka chini ya ulinzi wa
maombezi ya Mtakatifu Francisko Xaveri, akapona. Mara baada ya kupokea Sakramenti ya
Kipaimara na muujiza huu wa uponyaji kutoka kwa Mtakatifu Francisko Xaveri, Gaspar alianza
safari ya kuwa askari hodari wa Yesu Kristo.
Mtakatifu Gaspar kwa malezi bora na mwongozo imara toka kwa mama yake ulimsaidia kuwa
na tabia njema, ya utii, uvumilivu na unyofu. Aliweza kuthibiti hasira yake hata kusema “Sitaki
hasira hii, nakasirika kwa kuwa nimekasirika.” Daima alikuwa ni mtu wa sala, tafakari kufunga
na kujinyima ili kusaidia wahitaji. Katika kanisa la Yesu alikokuwa anasali, aliwasikiliza
wahubiri maarufu na aliporudi nyumbani alipanda juu ya meza na kuyarudia yote aliyokuwa
ameyasikia na kuyaona kule kanisani. Hakika huu ni moyo wa kimisionari wa kuwahubiria
mataifa yote.
Mwaka 1793 hadi 1797 Gaspari alipata elimu ya msingi na baadaye kujiunga na chuo ‘Roman
College’ kwa masomo ya sekondari na yale ya kitaalimungu. Alikuwa na bidii sana katika
masomo kwani alisema mmisionari anapaswa kuwa mtakatifu na msomi. Pamoja na masomo
chuoni alijitahidi kuabudu Ekaristi Takatifu kila siku ndipo alipochota nguvu ya ujasiri na
upendo. Muda wa mapumziko alikwenda kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa akisema;
“Twendeni tukajifunze hali na mahangaiko ya mwanadamu.” Watu walimwita mtakatifu mdogo.
Gaspar alipadrishwa, Julai 31, 1808. Kwa upadrisho wake alikuwa ni kama mafuta ya taa
yaliyomwagwa kwenye moto uwakao. Alifundisha Katekisimu kwa wengi ili wamjue na
kumtumikia Mungu. Pia alitembelea wagonjwa, wafungwa, maskini na watoto wa mitaani, na
alihubiri kwa ustadi mkubwa hata kuongoa mji wa Sonnino uliokuwa na majangili na waovu wa
kila aina. Gaspar alihuzuunika sana pale serikali ilipoamua kuuchoma moto mji wa Sonnino.
Lakini kwa jitahada za Gaspar watu wa mji huo walimrudia Mungu. Mafungo na mahubiri yake
yalielezwa kama “tetemeko la kiroho.”
Gaspar alikuwa mwaminifu daima kwa ahadi zake; akiwa ni kijana wa miaka 24 kwa ujasiri
alikataa kula kiapo cha utii kwa Mfalme Napolioni kinyume cha mwongozo wa Papa, akisema:
“Siwezi, Sipaswi na Sitaki.” Kwa ushujaa na Imani hii alikubali kwenda (kifungoni) kizuizini na
kuteswa, hakika Gaspar alikuwa nabii wa wakati wake. Gaspar alipotoka kifungo pamoja na
wenzake alitimiza ndoto yake ya kuaanzisha shirika. Tarehe 15 Agosti 1815, Shirika la
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu lilianzishwa katika konventi ya Mt. Felix huko Giano
karibu na Roma nchini Italia.
Kwa furaha Gaspar alisema: “Tumeweka Shirika hili chini ya ulinzi wa Mama Bikira Maria
Yeye atatuongoza kama Mama mwema.” Baba Mtakatifu Pius wa Saba akamkabidhi Padre
Gaspar na wenzake kazi ya kufufua maadili na imani ya watu waliojitenga na Kanisa kwa njia ya
mahubiri na mafungo. Gaspar alijitoa kwa moyo wote na kufanya kazi bila kujibakiza. Pale
wanashirika wenzake walipomshauri apumzike aliwajibu: “Kwa Mungu ni lazima tufanye
mengi, upesi na vizuri; mengi kwa sababu anastahili hivyo,upesi kwa sababu maisha ni mafupi,
na vizuri kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kumtumika Mungu.” Hakika Gaspari daima alijibu
kilio cha damu.
Kwa kazi nyingi Gaspar alizofanya afya yake ilizidi kudhoofika lakini alizidi kusisitiza
atapumzika mbinguni. Baada ya kuugua sana homa na maumivu makali alipokea kifo kwa furaha
akisema “ndiyo, ndiyo” akafariki Desemba 28, 1837. Alitangazwa Mtakatifu Juni 12, 1954 na
Papa Pio XII. Sikukuu ya Mt. Gaspar Del Bufalo huadhimishwa Oktoba 21 kila mwaka. Nia za
Mt. Gaspari…Zinaendelea….Hii ni kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei
ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu
duniani.
Makala hii imetayarishwa na Pd. INNOCENT E. MIKU wa Shirika la Wamisionari wa Damu
Azizi ya Yesu, (C.PP.S) Kanda ya Tanzania, kwa msaada wa vitabu: Damu ya Kristo Mto wa
Rehema,” “Mt. Gaspari Mtume wa Damu Takatifu ya Yesu,” “St. Gaspar Saint of The People”
na “The Herald of the Precious Blood St. Gaspar Del Bufalo.”


Kwa kusoma zaidi historia kwa kiingereza

                               BONYEZA HAPA


kwa ajili ya makala nyingine kuhusu dam azizi bofya hii picha







No comments